Thursday, December 1, 2016

KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W).

Tukio la kufishwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) mbele ya jamii ni jambo geni sana, kana kwamba katika historia ya ulimwengu tukio hili halikutokea. Ingawa tukio la kuzaliwa kwa Mtume Muhammad limepokelewa kwa nafasi kubwa isiyo kifani. Kwa hiyo, unaweza kuona hafla mbalimbali za kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) zikifanywa Misikitini, 

Madrasani, Majumbani, na katika Mazawia mbalimbali. Hili ni jambo jema sana, swali lilipo hapa ni, je, huyu afanyiwae haya yu hai mpaka sasa? Au amekwisha kufa? Ni kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) amekwisha kufa. 

Sasa, tarehe ya wafat wa Mtume, Waislamu wanaichukuliaje. Inafaa ikumbukwe tarehe hiyo ya wafat tarehe ambayo Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndiyo alioaga dunia, au haifai kuikumbuka?! Ilikuwaje! Maulamaa wa Kiislamu na Masheikh wa Twariqa katika tarehe zao za wafat hukumbukwa kwa visomo mbalimbali. 

Hili ni jambo jema, isipokuwa tarehe ya wafat wa Mtume Muhammad!!! Mtume (s.a.w.w) alipokaribia kufariki, kama ilivyopokewa na Ibn Abbas, alisema: “Nileteeni karatasi niwaandikie maandiko hamtapotea baada yake. Umar akasema Mtume anaweweseka. Katika riwaya nyingine, Umar akasema:

 “Hakika Mtume yamemzidi maradhi, na tunayo Qur’an inatutosha. Mara wakakhitilafiana (wako waliosema aletewe, na wako waliozuia) fujo likazidi. Mtume akawaambia: “Niondokeeni, na wala haipendezi kuzozana mbele yangu”.
Taz: Sahihi Bukhari:

Kitabul Itiswami bilkitabi wasunna, babu kara hiyatil khilafi.
Kitabul mardhaa, babu qawli quumuu anni.
Kitabun Nabi ila Kisra, babu maradhin Nabiyyi.
Kitabu Jihad, babu jawazil wafdi.
Kitabu IImi, babu kitabatil IImi.


Sahihi Muslim
Kitabul Waswiyya, babu tarkil waswiyya.

Kisha Mtume aliwaambia: “Niitieni Ali, Aisha akajibu: Laiti ungemwitisha Abubakar. Hafsa (naye) akasema: Laiti ungemwitisha Umar. (kila mmoja akawita baba yake) wakakusanyika mbele ya Mtume, Alipowaona Mtume akawambia: “Ondokeni nikikuhitajini nitakuiteni”.

Taz: Tarekhut Tabari J. 3 uk. 64
Mwana Aisha anasimulia kuwa: “Mtume alipougua maradhi aliyofia, aliamrisha Abubakar asalishe watu. Abubakar alipoingia Msikitini kutaka kusalisha, mara Mtume (s.a.w) akahisi woga, akatoka akiburuza miguu yake na huku ameshikiliwa na watu wawili (Ali na Abbas) alipoingia Msikitini, Abubakar akarudi nyuma ya safu, Mtume akakaa kuongoza swala.”

Taz: Tarekhut Tabari J. 3 uk. 64
Almuntadham J. 2 uk. 470


Katika riwaya hii, kuna mambo matatu yanahitaji kuangaliwa kwa kina:
Abubakar ni katika Maswahaba walioamriwa na Mtume kutoka pamoja na jeshi la Usama. Kwa hiyo, amma Abubakar alikwenda na jeshi kama Mtume alivyoamrisha, na kwa hiyo hakusalisha kwa sababu hakuwapo. Amma alikuwapo, kwa hiyo alipinga amri ya Mtume ya kwenda na jeshi, na kwa hiyo Abubakar amelaaniwa. 


Mtume (s.a.w.w) alipougua maradhi aliyofia: “Aitiwe Ali” tu, na wala si mtu mwingine. Na wapiga kampeni walipoita kila mmoja baba yake, Mtume aliwafukuza mbele yake, “ondokeni”. Mtume (s.a.w.w) amefariki akiwa kifuani kwa Ali bin Abi Talib ndani ya chumba cha Fatima (a.s). Anasema Imam Ali (a.s) kuwa: 

“Niliitwa na Mtume nikakaa naye karibu, nikampakata, akawa akininong’oneza kwa muda mrefu, mpaka mate ya Mtume yakanitiririkia!! Mtume (s.a.w.w) akakata roho akiwa kifuani kwangu!!!

Taz: Assiiratun Nabawiyya, ya Najahu Attai J. 2 uk. 316
At-Tabaqatul kubra J.2 uk. 26

Mtume (s.a.w.w) alivyotoka akichechemea taabani, na huku ameshikiliwa na watu wawili, Abubakar akapisha mahala hapo. Ni jambo gani lililomlazimisha Mtume kutoka akiwa hali hii, ikiwa yeye ndiye aliyeamuru kusalisha Abubakar? Ni kitu gani tena kilichomsonga kusalisha watu hali amekaa kwa taabu na dhiki kubwa? Kisha Mtume (s.a.w.w) akaagiza liandaliwe jeshi kupelekwa Rom. 

Mtume (s.a.w.w) akamteua Usama bin Zayd, kijana wa miaka kumi na saba au kumi na nane hivi aongoze jeshi hilo. Hii ni baada ya kumaliza hafla ya tukio kubwa lililotokea Ghadiir Khom ambapo Aya za Qur’an zilitemshwa, na Tamko la Mtume kutolewa na Waislamu wakatoa Baia yao kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s). 

 Mtume (s.a.w.w) akasisitiza Waislamu kujiandaa kutoka na jeshi hilo, akasema: “Andamaneni na jeshi la Usama, Mwenyezi Mungu amlaani atakaebaki nyuma”.
Taz: Afatu As-habil hadithi Uk. 12
Almilal wannihal J. 1 uk. 20


Katika Maswahaba walioamriwa na Mtume kutoka na jeshi la Usama ni Abubakar na Umar.
Taz: At- Tabaqatul kubra J. 2 uk. 190
Tarekhul Yaaquuby J. 2 uk. 113
Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 215
Almuntadhan J.2 uk. 458


Kitendo cha Mtume (s.a.w.w) cha kumtawalisha Usama bin Zayd katika jeshi hilo, kilipingwa vikali na maswahaba: “Amemtawalisha kijana mdogo juu ya Muhajirina na Ansar wakubwa wakubwa!” Baadhi ya maswahaba walisikika wakipinga. Khabari hii ikamfikia Mtume, akawatokea akiwa amefunga kitambaa kichwani, kwa maumivu makali ya kichwa aliyokuwa nayo, akawaambia: 

“Japokuwa mnashutumu kutawalishwa kwake (Usama) bila shaka mlikwisha shutumu kutawalishwa baba yake zamani. Na kwa hakika. Usama anafaa sana kwa uongozi, na baba yake alifaa kwa uongozi huo. Basi jiandaeni kwenda (na jeshi la) Usama, Mwenyezi Mungu amlaani atakaebaki nyuma”. Usama akatoka pamoja na kikundi kidogo cha jeshi, akapiga kambi nje ya mji wa Madina mahala paitwapo Jurf.
Taz: Siiratul Mustafa Uk. 685-686
Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 215
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 54-55


Je, ni maswahaba gani waliopinga uteuzi wa Mtume? Vipi waandishi wengi wa Tarekh wamejiziwia kutaja majina yao? Miongoni mwa maswahaba waliopinga uteuzi wa Mtume ni Abubakar bin Abi Quhafa! Alikataa kwenda na jeshi la Usama, na badala yake akaenda kwa mkewe Habiba bint Khaarija aliyoko kijijini Sunhi, (nje kidogo ya mji wa Madina) hakurudi mpaka alipojulishwa kuwa Mtume amefariki!!
Taz; Tarekh Ibn Athii J. 2 uk. 218
Assaqiifa, ya Najahu Attaai Uk. 172-176


Mtume (s.a.w.w) amefariki tarehe 28 Swafar siku ya Jumatatu mwaka wa kumi Hijria. Familia ya Mtume ikakusanyika tayari kwa mipango ya maziko. Umar bin Khattb kuona hivyo, akachukua upanga akawa akizunguka huku na kule katika eneo la Msikiti na nyumba ya Mtume. Umar kwa sauti yake ya juu akawa anaonya: 

“Wanafiki wanasema Mtume amekufa, na hakika Mtume hakufa, atakaesema Mtume amekufa nitakata shingo yake”. Mpaka alipofika Abubakar akitokea kijijini kwake Sunhi kwa mkewe, akaingia ndani alipolazwa Mtume (s.a.w.w). Alipotoka akasoma Aya: “Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume aliyepitiwa na Mtume kabla yake. Basi je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu? Na atakaerudi nyuma visigino vyake hatamdhuru kitu 

Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru”. 3:144. Umar akasema: “Wallahi, kana kwamba watu hawajui kuwa Ayah ii ilishuka kwa Mtume”. Kisha Abubakar na Umar wakaondoka kwenda kwenye ukumbi wa Bani Saaidah kwa ajili ya uchaguzi.
Taz: Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 219
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 67-69
Nurul absaar Uk. 57-59


Kumbuka, Umar anasema: “Wanafiki wasema Mtume amekufa”. Je, ni nani wanafiki? Nyumbani kwa Mtume kuna: Ali bin Abi Talib, Fatima bint Muhammad, Abbas bin Abdil Muttalib, Alfadhl bin Abbas, Qutham bin Abbas, na Usama bin Zayd. (ilipotangazwa kuwa Mtume amefariki, Usama pamoja na kikundi chake cha jeshi walirudi mjini) Hawa ndiyo waliokuwamo nyumbani kwa Mtume pamoja na mwili wa Mtume, na ndiyo waliotangaza kifo cha Mtume. Kwa mtazamo wa Umar, hawa ndiyo wanafiki, na ndiyo aliokusudia kukata shingo zao!!

Abubakar na Umar hawakuhudhuria osho wala maziko ya Mtume, walikuwa kwenye ukumbi wa Bani Saaidah wakichaguana!!
Taz: Kanzul Ummal, kitabul khilafa maal-imaara khilafatu Abibakar
Almuswannaf, ya Ibn Shayba, babul Maghaz khilafatu Abibakar
Kama ambavyo, Mwana Aisha (mkewe Mtume) hakuhudhuria osho wala maziko ya Mtume, alipotea nyumbani kwa Mtume siku mbili, mwenyewe Mwana Aisha anasimulia hapa: “Wallahi hatukuelewa maziko ya Mtume mpaka tuliposikia kelele za majembe usiku wa Jumanne (wakati wakichimba kaburi):
Taz: Al-muntadham J. 2 uk. 482


Asiiratun Nabawiyya, ya Najah Attaai J. 2 uk. 314
Assunanul Kubra J. 3 uk. 574Tarekhut Tabari J. 3 uk. 81
Kifo cha Mtume kinatatanisha, je, amekufa kifo cha kawaida au ameuliwa kwa sumu? Anasema Mwana Aisha kuwa: “Tulimnywesha dawa Mtume wakati wa maradhi yake, na Mtume akiwazuia: “Msininyweshe”.

Taz: Tarekhut Tabari J. 3 uk. 62
Fat-hul Baary J.10 uk. 17


Waandishi wa kiislamu wanasema kuwa: “Waliohusika kumnywesha dawa hiyo kwa nguvu ni Aisha na Hafsa (wakeze Mtume) na kwamba dawa hiyo ni sumu!!
Taz: Assiiratun Nabawiyya, ya Najahu Attaai J. 2 uk. 379
Alburhan fyilafsiril Quran J. 2 uk. 117
Tafsirul ‘Ayyaashy J. 1 uk. 224
Tafsirus Saafy J. 1 uk. 389-390


Mtume (s.a.w.w) alikoshwa, kuswaliwa, kuzikwa na: Ali bin Abi Talib, Abbas bin Abdul Muttalib, Qutham bin Abbas, Alfadhlu bin Abbas, na Usama bin Zayd. Mtume (s.a.w) amezikwa siku ya Jumatatu, amepewa Utume siku ya Jumatatu, amehama Makka kwenda Madina siku ya Jumatatu, amefika Madina siku ya Jumatatu, na amefariki siku ya Jumatatu.
Taz: Almuntadham J. 2 uk. 477
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 80

Imetolewa na:
Sheikh Rajabu Shaban Kabavako

MSAJILI WA HAZINA ATOA UFAFANUZI KUHUSU KUKAUKA FEDHA KATIKA MZUNGUKO, PAMOJA NA SABABU ZA MABENKI MENGI KULALAMIKA KUFILISIKA

 
Msajili  wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru amesema benki nchini zinashindwa kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba madai ya kuwa hali zao ni mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha zake zitunzwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hazina ukweli.

Mafuru amesema taarifa ambazo serikali wanazo ni kwamba benki hizo zaidi ya 50 zimekopesha fedha nyingi kwa watu mbalimbali, lakini marejesho ya madeni hayo yamekwama kiasi cha kusababisha benki hizo ziwe katika hali hiyo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Msajili wa Hazina licha ya kukiri kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua kwamba fedha inazozipata zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya matumizi ya kawaida, benki zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha ilizokopesha watu na taasisi mbalimbali.

Akizungumzia taarifa zinazoenezwa kwamba benki zimekosa fedha za kujiendesha, Mafuru alisema taarifa walizozipata ni kwamba Septemba mwaka huu, benki hizo zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya Sh trilioni 16.3 kwa watu mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.43 zimekopeshwa bila ya kurudishwa katika benki husika na kwamba benki hizo zinashindwa kueleza ukweli uliopo badala yake wanalalamika kwamba hatua ya serikali kuamua fedha zake zitunzwe BoT badala ya katika benki za kibiashara, ndio sababu ya hali yao (benki) mbaya.

Kwa mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua uamuzi huo wa kuzitoa fedha zake kutoka katika benki mbalimbali za kibiashara nchini kwa ajili ya kuwezesha serikali kujua mapato wanayopata kutoka katika taasisi zake.

Msajili wa Hazina amesema zaidi ya Sh bilioni 515 zimeingizwa BoT baada ya uamuzi huo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao ulitangazwa na Rais John Magufuli baada ya kushika madaraka mwaka mmoja sasa. 

Mafuru alikiri kuwa ni kweli kwamba mzunguko wa fedha umekuwa mdogo na kueleza kuwa chanzo chake si kwamba benki zimekosa fedha kwa ajili ya kujiendesha.

Alifafanua kuwa awali watu wengi walitegemea safari na posho ambazo baada ya chenji kubaki, walikuwa wakitumia bila ya malengo, lakini sio kwamba mzunguko huo wa fedha unawaathiri watu wote.

“Tumeona tusitegemee wahisani badala yake tujiwekeze katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa sasa haitaonekana, lakini baadaye itasaidia kuondoa nafasi iliyopo sasa,’’ alisema Mafuru.

“Tayari shilingi bilioni 515 zimeingizwa BoT na mpaka Septemba mwaka huu fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti hiyo. BoT ni sehemu ya mfumo wa benki, kwani itakuwa inafanya kazi ya kukopesha kama zilivyo benki nyingine,” alifafanua Mafuru ambaye ofisi yake inasimamia mashirika na taasisi za umma.

Alifafanua kuwa ofisi yake ambayo ina jukumu la kusimamia mapato na matumizi, awali walikuwa wanapata shida kupata taarifa za mapato na matumizi katika benki hizo zilizopo kila kona nchini na kwamba baada ya BoT kuchukua dhamana hiyo, imewasaidia, kwani wanaandika barua na kupatiwa taarifa hizo kwa muda mfupi.

Alisema serikali inategemea mapato yake kutoka katika makundi matatu ambayo ni Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na kupitia mashirika na taasisi mbalimbali.

Alisisitiza kuwa itasaidia kujua mashirika hayo zaidi ya 260 namna wanavyotumia fedha zake katika miradi mbalimbali na kwamba suala la kuchukua fedha bila ya kuzitumia lisiwepo.